Apr 07, 2021 10:45 UTC
  • Ajali ya barabarani yaua 14 na kujeruhi wengine wengi Malindi, Kenya

Ajali mbaya iliyotokea mapema leo katika barabara kuu ya Malindi-Mombasa imesababisha vifo vya watu wasiopungua 14 na kujeruhi wengine wengi.

Ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Kwa Shume karibu na Kizingo, Kaunti ya Kilifi, imehusisha basi la kampuni ya usafiri na uchukuzi ya Muhsin na basi la Sabaki T Shuttle.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Bw Kutwa Olaka aliyezuru eneo la mkasa, amesema basi la Muhsin lilikuwa likielekea Garsen kutoka Mombasa, huku lile la Sabaki T Shuttle likielekea Mombasa kutoka Malindi.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa moja asubuhi leo Jumatano.

Abiria 18 walipata majeraha mabaya, na wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.

“Tumelaza watu 18 ambapo sita kati yao wako katika hali mahututi,” amesema mkuu wa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi, Dkt Joab Gayo.

Gayo ameongeza kuwa, 14 kati ya majeruhi hao18, ni wa jinsia ya kiume na wanne ni wa jinsia ya kike.

Watu 14 wameuwa katika ajali hiyo.

Wengine waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali za Tawfiq na Star, zote zikiwa za wamiliki binafsi, mjini Malindi kwa ajili ya kupewa matibabu.

Madereva wa mabasi hayo walifariki dunia papo hapo.

Mojawapo ya mabasi hayo lilikuwa na wafanyakazi kadha wa serikali ya Kaunti ya Kilifi.

Miili ya walioaga dunia ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.