Apr 08, 2021 13:08 UTC
  • Uganda na Misri zimetia saini mapatano ya ushirikiano wa kijeshi

Uganda na Misri zimetia saini mapatano ya ushirikiano wa mabadilishano ya taarifa za siri za kijeshi huku mgogoro baina ya Misri na Ethiopia ukiendelea kushadidi kutokana na hatua ya Ethiopia kuendelea kujaza maji katika bwawa lake la Mto Nile.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF), mapatano hayo yalitiwa saini Jumatano baina ya Mkuu wa Intelijensia ya Kijeshi katika UPDF na Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Misri.

Afisa wa intelijensia katika Jeshi la Misri ambaye aliongoza ujumbe wa nchi yake katika mazungumzo ya Kampala Meja Jenerali Sameh Saber El-Degwi, amesema kwa kuzingatia kuwa Uganda na Misri ni nchi ambazo zinamatumizi ya pamoja ya Mto Nile, ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni jambo lisiloepukika kwa sababu kile ambacho kinawaathiri watu wa Uganda pia kinawaathiri watu wa Misri.  Uganda ambayo ni chimbuko la Mto Nile imekuwa ikipinga hatua yoyote ya Misri kudhibiti kikamilifu masuala ya Mto Nile. Kwa mujibu wa mapatanoo hayo mapya, nchi hizo mbili sasa zitakuwa zikibadilishana taarifa za siri za kijeshi mara kwa mara.

Mapatano hayo yamesainiwa huku Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri akiwa ameionya Ethiopia kuhusu kutokea vita baina ya nchi hizo mbili iwapo Addis Ababa itaendelea kushirikilia msimamo wake wa kuingiza maji katika bwawa la al Nahdha.

Aidha amesisitiza kwamba nchi yake na Sudan zina msimamo wa pamoja kikamilifu kuhusu bwawa la al Nahdha na wana ushirikiano mzuri zaidi katika suala hilo kuliko masuala mengine yote.

Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri ametoa onyo la kuishambulia kijeshi Ethiopia katika hali ambayo mazungumzo ya pande tatu za Misri, Ethiopia na Sudan huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamemalizika bila ya kufikia utatuzi wa mgogoro huo wa bwawa la al Nahdha la nchini Ethiopia.

Serikali ya Addis Ababa inasema ni haki yake kutumia rasilimali ya nchi yake na kwamba bwawa la al Nahdha limejengwa nchini Ethiopia kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi na kuzalisha umeme. Hata hivyo viongozi wa Misri na Sudan wana wasiwasi mkubwa kwamba bwawa hilo litapunguza kiwango cha maji yanayohitajiwa na nchi hizo mbili kutoka Mto Nile.