Apr 08, 2021 13:12 UTC
  • Jeshi la Somalia lachukua udhibiti wa ngome za magaidi wa al-Shabab

Jeshi la Somalia (SNA) limetangaza kuchukua udhibiti wa kambi kadhaa za kundi la kigaidi la al-Shabab huko Galgaduud, katikati mwa Somalia.

Mafanikio hayo yamejiri  katika operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi hilo la magaidi wakufurishaji. Kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Somalia Mohamed Tahlil Bihi amesema, wanajeshi wameteka kambi mpya katika maeneo ambayo ni ngome za al-Shabab na kusababisha vifo na majeruhi wengi kwa kundi hilo.

Operesheni hiyo imefanywa baada ya jeshi hilo kukomboa maeneo ya Sinadhaqqo na Labi Dulle wiki iliyopita huko Galgaduud ambapo magaidi wengi waliuawa na silaha zilikamatwa.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 baada ya kuangushwa utawala wa Siad Barre. Katika miaka ya  hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hata hivyo pamoja na jitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeleza hujuma Somalia na katika nchi jirani ya Kenya.

 

Tags