Apr 11, 2021 04:16 UTC
  • Profesa Assad wa Tanzania awalaumu wanaounga mkono wakuu wa nchi bila kuhoji

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa zamani wa Tanzania,  Profesa Mussa Assad amewalaumu vikali wale viongozi ambao wanaunga mkono bila ya kuhoji lolote linalosemwa na wakuu wa nchi na amewaita ni watu wanaosaka nafasi na fursa tu serikalini.

Aidha Profesa Assad amesema, asilimia 60 ya viongozi walioko serikalini hivi sasa huko nchini Tanzania hawafai na amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuanza na safu mpya  ya viongozi serikalini, akisisitiza kuwa, waliopo wengi hawana uwezo mzuri kiutendaji.

Profesa Assad alisema hayo jana Jumamosi Aprili 10, 2021 wakati wa uzinduzi wa mfululizo wa midahalo kwa umma itakayokuwa ikiandaliwa na Chuo Kikuu cha Waislamu cha  Morogoro (MUM).

Amesema kwa mtazamo wake asilimia 60 au 50 ya viongozi ndani ya Serikali si wazuri, hivyo  wanapaswa kupumzishwa ili mambo yaanze upya.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa zamani wa Tanzania, Profesa Mussa Assad

 

Amesema: “Inapofika mahali unaona mtu anakosea na huwezi kusema kama mtu anakosea, unakuwa umefika mahali pabaya sana. Si lazima umkosoe wazi wazi,  lakini angalau basi andika kwamba mheshimiwa nimeona umefanya jambo hili na hili, lakini nafikiri kimsingi jambo hilo halikuwa sawa."

Profesa Mussa Assad pia amesema watu wenye tabia ya kuunga mkono kila kitu na kila wakati bila ya kuhoji, hao ni wasaka fursa na hawana msaada wowote katika nchi.

Ametoa mfano kwa kusema: "Kuna watu waliunga mkono na sasa wanaunga mkono tena vitu ambavyo haviendani, hao ni wasaka fursa tu na kawaida yao hawatusaidii chochote, nchi inahitaji watu wenye fikra tunduzi ambao wakati ule walisema kitu kile na sasa wanasema vilevile na wataendelea kufanya mambo sahihi. Wanaangalia upepo unaendaje, wakati ule walikuwa wanashadadia mambo yakifanywa hata bila kufuata taratibu za kisheria na sasa wanashadadia hata mambo ambayo yanatofautiana na yale."