Apr 11, 2021 14:39 UTC
  • Sudan: Jamii ya Kimataifa iingilie kati kabla vita havijatokea kwa sababu ya bwawa la An-Nahdhah

Afisa mmoja wa serikali ya Sudan amesema, jamii ya kimataifa inapaswa iingilie kati kwenye kadhia ya bwawa la An-Nahdhah kabla ya kutokea vita vikali kwa sababu ya mzozo wa maji.

Kwa mujibu wa tovuti ya Araby21, Tahir Abu Haajah, mshauri wa masuala ya habari wa Abdel Fattah al-Burhani, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan ametahadharisha juu ya kutokea vita baina ya Ethiopia, Misri na Sudan juu ya suala la maji na akaeleza kwamba, vita vya kugombania maji na Ethiopia vinaweza kuwa na maafa makubwa kuliko inavyofikiriwa.

Indhari ya afisa huyo wa serikali ya Sudan inatolewa huku Ethiopia ikiwa imeshikilia msimamo wake wa kuanzisha awamu ya pili ya ujazaji maji katika bwawa lake la An-Nahdhah.

Misri pia, imelikataa pendekezo la Ethiopia la kutoa taarifa ya pamoja kuhusu utekelezaji wa awamu ya pili ya ujazaji maji katika bwawa hilo.

Jumatano iliyopita, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri alionya kuhusu uwezekano wa kutokea vita kati ya nchi yake na Ethiopia baada ya mazungumzo juu ya suala hilo kumalizika bila ya kuwa na tija. El Sisi alisema, Misri na Sudan zinaendelea na mashauriano na kwamba machaguo yote ya uchukuaji hatua yako mezani.

Kikao cha mawaziri wa maji wa Misri, Sudan na Ethiopia kilichofanyika Jumanne iliyopita mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuainisha haki ya kila nchi katika maji ya Mto Nile na kuanza kwa awamu ya pili ya ujazaji maji ya mto huo kwenye bwawa la Ethiopia la An-Nahdhah kilimalizika bila kufikiwa makubaliano…/