Apr 12, 2021 08:10 UTC
  • Sudan: Endapo tutaingia katika vita na Ethiopia tutaibuka na ushindi

Mjumbe wa Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan ametangaza kuwa, endapo nchi yake itaingia katika vita na Ethiopia basi itaibuka na ushindi.

Luteni Jenerali Yassir al-Atta amesema kuwa, Sudan haitalegeza kamba kuhusiana na maeneo ya al-Fushqa ambayo yanagombaniwa na nchi hiyo na Ethiopia kwani maeneo hayo ni sehemu ya ardhi ya Sudan.

Mjumbe huyo wa Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan amesisitiza kuwa, nchi yake haina nia ya kuingia katika vita na Ethiopia, lakini kama italazimika na kuingia vitani basi Khartoum itaibuka na ushindi.

Luteni Jenerali Yassir al-Atta ameongeza kuwa, Sudan itaibuka na ushindi katika vita hivyo kwa kuwa ipo katika haki.

Hivi karibuni viongozi wa Sudan walichukua uamuzi wa kukifunga kivuko cha mpakani kati ya nchi hiyo na Ethiopia.

 

Viongozi wa Sudan wanasema kuwa, wameamua kukifunga kivuko hicho cha mpakani kati ya nchi hiyo na Ethiopia baada ya kujiri mapigano kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo na kundi moja la wanajeshi wa Sudan. 

Sudan na Ethiopia zinahitilafiana kuhusu eneo la ardhi ya kilimo huko al Fushqa linalopatikana katika mpaka wa kimataifa wa Sudan; eneo ambalo wakulima wa Kiethiopoa wanaishi hapo kwa muda sasa.  

Wasiwasi katika mpaka wa Sudan na Ethiopia uliongezeka baada ya kutokea mapigano katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana (2020).

Tags