Apr 12, 2021 12:11 UTC
  • Rais Samia Suluhu na Mzee Mwinyi
    Rais Samia Suluhu na Mzee Mwinyi

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili nchini Tanzania, Dkt. Ali Hassan Mwinyi leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye amempongeza kwa kuanza vizuri majukumu yake ya kuongoza nchi.

Akizungumza baada ya mazungumzo yao, Rais mstaafu Mwinyi amesema amefika nyumbani kwa Rais Samia kumjulia hali, kumtia moyo na kumhakikishia kuwa yeye na wazee wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano na kumsaidia wakati wowote watakapohitajika kufanya hivyo.

“Mama ameanza vizuri, ingekuwa ni nyimbo ningesema once more!!!, ameanza vizuri kabisa na kila mmoja ana furaha. Kila raia unayemsikia anasema Mama ameanza vizuri. Tuliyekuwa nae tulikuwa na Rais mzuri sana, mzoefu wa mambo ya kiserikali”, amesema Mzee Mwinyi.

Mzee Mwinyi akizungumza na Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia kwa kuacha balaa, ugomvi na fitina badala yake wawe na umoja, mshikamano na kufanya juhudi za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Ali Hassan Mwinyi alikuwa rais wa Tanzania baada ya kuondoka madarakani rais wa kwanza wa nchi hiyo, Julius Kambarage Nyerere. Aliingoza nchi hiyo kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1985 hadi 1995. 

Tags