Apr 13, 2021 02:50 UTC
  • Rais wa Zanzibar 'awatumbua' Makamanda wakuu watatu wa Idara Maalum za SMZ

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Makamanda watatu wa Idara Maalum za SMZ.

Waliotenguliwa ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Ali Mtumweni Hamad na Mkuu wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Comodore Hassan Mussa Mzee.

Akitoa taarifa maalum kwa wananchi kupitia vyombo vya habari Ikulu Jijini Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema, kufuatia taarifa za uwepo wa wafanyakazi hewa katika Idara Maalum za SMZ, aliunda kamati ya uchunguzi ya kufanya uhakiki wa idadi ya wafanyakazi pamoja na viwango vya mishahara vinavyotolewa kwa vikosi vyote.

Akitoa taarifa kwa umma juu ya ripoti ya Kamati ya Uhakiki iliyomfikia, Rais wa Zanzibar amesema, kulikuwa na watumishi 381 waliokuwa wakilipwa mishahara bila ya kuwa katika utaratibu unaotakiwa, ikiwa na maana kwamba hao ni watumishi hewa.

Dk Mwinyi ameongeza kuwa, waliwahi kukamatwa baadhi ya maafisa katika nyumba ya mtu binafsi wakiwa wamewavisha sare za Jeshi vijana na kuwapiga picha ili kuthibitisha kwamba wamo katika ajira rasmi. 

Rais wa Zanzibar aidha amesema, imebainika kwamba fedha zilizotumika kwa upotevu ni kiasi cha Shilingi Bilioni mbili, milioni mia mbili thelathini na tatu, laki saba na ishirini na tano kutokana na fedha zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hao hewa.

Rais Dk Hussein Mwinyi (kulia) na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, walioasisi maridhiano mapya ya kisiasa baada ya uchaguzi wa Zanzibar

Utenguzi huo umefanyika sambama na malalamiko yaliyoibuka hivi karibuni juu kile kilichotajwa kama 'hujuma' zilizofanywa na vikosi vya SMZ kwa lengo la kuvuruga chaguzi ndogo za uwakilishi na udiwani zilizofanyika katika visiwa Zanzibar.

Wadadisi wa siasa za Zanzibar wanasema, fagio la chuma la Rais Mwinyi lililowasomba makamanda hao wakuu wa vikosi vya Idara Maalum ya SMZ huenda limehusisha pia shutuma hizo za kuingilia uchaguzi wa udiwani wa jimbo la Kinuni Unguja na ule wa uwakilishi katika jimbo la Pandani kisiwani Pemba, hatua ambayo imetafsiriwa kama njama ya kuyavuruga maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya vyama vya CCM na ACT-Wazalendo kufuatia machafuko yaliyozuka wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.../

 

 

 

 

 

Tags