Apr 14, 2021 03:17 UTC
  • Kiongozi wa waasi wa Tuareg wa nchini Mali, auawa kwa risasi

Kiongozi wa waasi wa Tuareg ameuawa kwa majeraha ya risasi aliyoyapata baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake jana Jumanne, Aprili 13, 2021, mjini Bamako. Msemaji wa muungano wa waasi hao wa Tuareg pamoja na msemaji wa serikali ya Mali wamethibitisha mauaji hayo.

Msemaji wa waasi hao, Almou Ag Mohamed amesema, Sidi Brahim Ould Sidati, mkuu wa Harakati ya Uratibu wa Watu wa Azawad (CMA) alipigwa risasi jana Jumanne nje ya nyumba yake, huko Bamako, mji mkuu wa Mali. Ameongeza kuwa, Sidati alipelekwa haraka hospitalini lakini amefariki dunia kwa majeraha hayo ya risasi.

Serikali ya Mali nayo imethibitisha habari hiyo na kusema kuwa Sidati ameuawa kwa majeraha ya risasi na kwamba serikali itaanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo. Hadi inatangazwa habari hiyo hakuna kundi wala mtu yeyote aliyetangaza kuhusika na mauaji hayo.

Makundi hasimu yalitia saini makubaliano ya amani mwaka 2015 ili kumaliza mapigano nchini Mali

 

Sasa hivi nchi ya Mali ya magharibi mwa Afrika imo kwenye kipindi cha mpito kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana. Mauaji ya kiongozi wa waasi wa Tuareg yataharatisha utekelezaji wa makubaliano ya amani ambayo kiongozi huyo aliyatia saini mwaka 2015 kwa niaba ya muungano wa waasiwa wa CMA.

Muungano huo ni wa waasi wanaopigania utawala wao katika eneo la jangwani la kaskaizni mwa Mali ambalo wanaliita Azawad. Kwa muda mrefu watu wa eneo hilo ambao ni wa kabila la Touareg wanailalamikia serikali ya Mali kwa kuwadhulumu na kuwapuuza kupindukia.

Muungano huo wa waasi ni miongoni mwa pande zilizotia saini makubaliano ya amani mwaka 2015 pamoja na serikali na muungano wa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Mali. Makubaliano hayo yalifikiwa ili kumaliza miaka mingi ya ukosevu wa utulivu, mapigano, mashambulizi na mlolongo wa mapinduzi ya kijeshi na mabadiliko ya kisiasa na kikatiba.