Apr 14, 2021 08:15 UTC
  • Ethiopia yaomba msaada wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuwaondoa wanajeshi wa Sudan katika ardhi yake

Serikali ya Ethiopia imeiomba jamii ya kimataifa iishinikize serikali ya Sudan kwa ajili ya kuwaondoa wanajeshi katika ardhi ya nchi hiyo inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema kuwa, Inasikitisha kuona kuwa, Sudan inahatarisha usalama wa eneo la Pembe ya Afrika kwa kushambulia ardhi ya Ethiopia, kupora na kuwalazimisha raia wakimbie makazi yao na vilevile kupiga ngoma za vita kwa ajili ya kukalia kwa mabavu ardhi zaidi ya Ethiopia.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Ethiopia iko tayari kutatua mzozo wa mpaka na Sudan kwa kutumia vigezo vya hati ya utatuzi wa mizozo ya mwaka 1972. Hati hiyo ilipiga marufuku kuwafukuza raia katika makazi yao na kutumia mabavu kwa ajili ya kutatua mizozo ya mpakani.

Wanajeshi wa Sudan hivi karibuni walipigana kwa mara kadhaa na wenzao wa Ethiopia; huku kila upande ukishambulia maeneo ya upande wa pili.  

Sudan na Ethiopia zinahitilafiana kuhusu eneo la ardhi ya kilimo huko al Fashaga linalopatikana katika mpaka wa kimataifa wa Sudan; eneo ambalo wakulima wa Kiethiopoa wanaishi hapo kwa muda sasa.  

Wakati huo huo Khartoum inalituhumu jeshi la Ethiopia kuwa linauwanga mkono na kuwasaifia wanamgambo wa Kisudani.