Apr 14, 2021 11:29 UTC
  • Umoja wa Mataifa waitaka serikali ya Uganda iheshimu haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka serikali ya Uganda isitishe mara moja kile ilichokitaja kuwa, ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani ambao ulianza kabla ya uchaguzi mkuu wa Januari mwaka huu ulioleta mzozo na unaendelea kuwakandamiza wafuasi wa upinzani.

Wataalamu hao wanasema kuwa, wana wasiwasi mkubwa na ripoti zinazotolewa za kuweko ukandamizaji ulioenea na unaoendelea dhidi ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao.

Ripoti zinaeleza kuwa, zaidi ya watu 50 wameuawa kwa njia za kikatili zinazotumiwa na vikosi vya usalama, pamoja na matumizi ya risasi za moto zilizofyatuliwa bila tahadhari, na watu wengine wasiopungua 20 wamepoteza maisha katika visa vinavyohusiana na matukio ya uchaguzi.

Rais Yoweri Kaguta Museveni ambaye serikali yake inatuhumiwa kwamba, inakandamiza wapinzani

 

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamezitaka mamlaka husika nchini Uganda zifanye uchunguzi mara moja na kwa kina kuhusiana na matukio hayo yakiwemo madai ya mauaji ya kiholela, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kiholela, watu kutoweka, kuteswa na kutendewa mambo mabaya, kunyimwa haki ya mchakato unaofaa wa kisheria na kubinywa uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

Kukamatwa kiholela na kuwekwa kwenye kifungo cha nyumbani kati ya tarehe 14 na 25 Januari 2021 kwa  kiongozi mashuhuri wa upinzani Bobi Wine, ambapo mahakama Kuu iliamua kuwa ni kinyume cha katiba, ni dalili ya mbinu kali za kukandamiza za upinzani na kutokuwepo kwa haki katika mchakato wa sheria, wamesisitiza wataalamu hao wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.