Apr 16, 2021 03:34 UTC
  • Amnesty: Jeshi la Eritrea linaendelea kuua raia Tigray, Ethiopia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amesty International limesema jeshi la Eritrea lingali linaua raia katika eneo la Tigray, wiki chache baada ya Ethiopia kutangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo jirani yake wameanza kuondoka katika eneo hilo linalokumbwa na mgogoro na mapigano kwa miezi kadhaa sasa.

 Amnesty imesema mauaji ya Jumatatu ya wiki hii katika mji wa Adwa ni mfano hai wa mwendelezo wa ukatili unaofanywa na wanajeshi wa Eritrea dhidi ya raia wa Ethiopia katika eneo la Tigray.

Sarah Jackson, Mkurugenzi wa kieneo wa Amnesty International amesema wanajeshi wa Eritrea waliokuwa wakipita katika mji huo, walianza kuwamiminia risasi raia koholela, ambapo watatu miongoni mwao waliuawa, huku wengine 19 wakijeruhiwa.

Jackson ameongeza kuwa, mauaji hayo ni shambulio jingine lililo kinyume cha sheria cha wanajeshi wa Eritrea dhidi ya raia ndani ya ardhi ya Ethiopia. 

Mapema mwezi huu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia ilisema wanajeshi wa Eritrea waliovuka mpaka na kuingia nchini humo baada ya kuchochewa na harakati ya TPLF wameanza kuondoka; na kwamba wanajeshi wa Ethiopia wamechukua udhibiti wa mpaka wa kitaifa.

Mgogoro wa wakimbizi kutokana na mapigano Tigray

Mwezi uliopita, Human Rights Watch (HRW) ilisema  wanajeshi wa Eritrea wameua mamia ya raia wakiwemo watoto wadogo katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Mbali na maelfu ya watu kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao huko kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo baina ya wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea kwa upande mmoja, na harakati ya kupigania ukombozi wa eneo la Tigray TPLF kwa upande mwingine. 

Tags