Apr 16, 2021 03:34 UTC
  • Serikali ya mpito ya Mali yatangaza tarehe ya uchaguzi mkuu

Serikali ya mpito ya Mali imetangaza Februari 27 mwaka ujao 2022 kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita mwaka jana.

Utawala huo wa mpito ulitangaza hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, uchaguzi wa rais na bunge utafanyika Februari 27 mwakani, na kwamba duru ya pili ya uchaguzi wa rais itafanyika Machi 20 mwaka huo, iwapo hakuna mgombea wa urais atapata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza.

Ratiba hiyo ya uchaguzi iliyotolewa jana na serikali ya mpito ya Mali inaonesha kuwa, taifa hilo la magharibi mwa Afrika litafanya kura ya maoni Oktoba 31 mwaka huu 2021.

Sasa hivi nchi ya Mali imo kwenye kipindi cha mpito kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana. Mapinduzi hayo ya kijeshi nchini Mali yalitokea mwezi Agosti mwaka jana, ambapo Rais Ibrahim Boubacar Keita na Waziri Mkuu wake, Boubou Cissé walitiwa mbaroni na wanajeshi waasi.

Keita aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi Mali

Masaa machache baada ya kukamatwa, Keita alijitokeza katika televisheni ya taifa na kutangaza kujiuzulu huku akisisitiza hataki kubakia kwake madarakani kuwe chanzo cha umwagikaji damu nchini humo. Bah Ndaw kanali mstaafu na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Mali Septemba mwaka jana aliapishwa kuwa Rais wa kipindi cha mpito nchini humo. 

Rais huyo wa kipindi cha mpito alikubali kuiongoza Mali kwa muda usiopungua miezi 18 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, kutokana na vikwazo na mashinikizo ya jumuiya za kieneo kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).