Apr 16, 2021 04:34 UTC
  • Mwongozo wa ustawi wa biashara ya kilimo Afrika wazinduliwa

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, na Idara ya Kilimo, Maendeleo Vijijini, Uchumi wa Bahari na Maendeleo Endelevu ya Muungano wa Afrika, AUC-DARBE, zimezindua mwongozo wa kukuza biashara ya kilimo miongoni mwa mataifa ya Afrika chini ya makubaliano mapya ya Eneo la Biashara Huru barani humo, AfCFTA.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na FAO na AU, Mfumo wa Kukuza Biashara baina ya Afrika katika Bidhaa na Huduma za Kilimo uliozinduliwa jana Accra, Ghana  ni mwongozo wa kupanua biashara ya kilimo miongoni mwa nchi za Kiafrika na unakusudia kufungua uwezo wa sekta ya kilimo kuchangia ukuaji endelevu na jumuishi. 

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa FAO ambaye pia ni Mwakilishi wa Kanda ya Afrika Abebe Haile-Gabriel, Kamishna wa Muungano wa Afrika, Josefa Sacko, na Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Mene kwa pamoja katika utangulizi wa chapisho la mwongozo, wamesema, "mfumo huo unatoa kichocheo cha wakati unaofaa kwa mabadiliko bora zaidi, mifumo shirikishi ya kilimo-chakula, inayojumuisha, thabiti na endelevu, maendeleo endelevu na ustawi barani Afrika. Kipaumbele muhimu ni kufuata sera na mipango ya mabadiliko ya viwanda ambayo inasaidia sekta binafsi kuongeza thamani kwa bidhaa za kiafrika zinazouzwa nje, kushindana na uagizaji kutoka nje ya Afrika na kupanua fursa za kuzalisha kazi."

Taarifa pia imeeleza kuwa Afrika ni eneo linaloagiza bidhaa za kilimo na chakula kutoka nje zenye thamani ya dola bilioni 80 kila mwaka, kama vile nafaka, nyama, bidhaa za maziwa, mafuta na sukari. Ni sehemu ndogo ya jumla ya biashara ya kilimo barani Afrika iliyo miongoni mwa nchi nyingine za Kiafrika. Biashara ya kilimo ndani ya Afrika inakadiriwa kuwa chini ya asilimia 20.

Biashara katika eneo la soko huru barani Afrika, AfCFTA ilianza mnamo Januari mosi mwaka huu wa 2021 na ndio eneo kubwa zaidi la biashara huria ulimwenguni kulingana na idadi ya nchi zilizomo. AfCFTA inawakilisha soko la watumiaji bilioni 1.2.

 

Tags