Apr 16, 2021 07:56 UTC
  • Ongwen aiambia ICC hakuwa na uwezo wa kusitisha mauaji Uganda

Dominic Ongwen Kamanda wa zamani wa kundi la waasi wa LRA nchini Uganda amezungumza mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na kusema hakusimamia jinai zozote na hakuwa na uwezo wa kuzisitisha.

Akizungumza katika kikao cha ICC Alhamisi mjini The Hague, Uholanzi, Ongwen amesema hataomba msamaha kwa sababu hakutenda jinai anazotuhumiwa kutenda.

Kundi la waasi wa Kikristo wa LRA wanaoongozwa Joesph Kony wamekuwa wakitekeleza jinai kaskazini mwa Uganda kwa zaidi ya miaka 20 kwa lengo la kuindoa madarakani serikali ya Rais Museveni. Waasi hao ambao wamepanua wigo wao hadi katika nchi jirani sasa wamedhoofika na wanakaribia kuangamizwa kikamilifu.

Ongwen ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa Uganda, LRA, amefikishwa mbele ya mahakama ya ICC, ambayo ilimpata na hatia mwanzoni mwa mwezi wa Februari ya makosa 61 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa kaskazini mwa Uganda kati ya mwaka 2002 na 2005.

Kinara wa LRA Joseph Kony

Ogwen aliyekamatwa mwaka 2015 alieleza jinsi alivyotekwa nyara na wapiganaji wa Joseph Kony mnamo mwaka 1987 alipokuwa akienda shule. Pia amesimulia Jinsi, baada ya jaribio la kutoroka, alipewa panga, na kuua wafungwa, akilazimishwa kunywa damu yao na kula matumbo yaliyochanganywa na maharagwe. ICC inatazamiwa kutoa hukumu ya Ongwen mnamo Mei 6 na akipatikana na hatia atafungwa miaka 30 jela