Apr 16, 2021 12:05 UTC
  • UN: Eritrea ikomeshe ukatili na mauaji Tigray

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, askari wa Eritrea wanapaswa kukomesha ukatili na vitendo viovu katika eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuondoka mara moja katika eneo hilo.

Mark Lowcock ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, raia wa kawaida wanaendelea kuaga dunia katika eneo hilo kutokana na njaa na kwamba hali ya mambo katika eneo hilo inaendelea kuwa mbaya zaidi. Amesema wahalifu katika eneo hilo la Tigray Kaskazini wanatumia ukatili wa kubaka wanawake kama silaha ya vita. 

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa idadi ya watu waliokimbia makazi yao katika jimbo hilo la Tigray imeongeze na kufikia zaidi ya watu milioni 1.7. Amesema watu 9 kati ya kila wakazi kumi wa Tigray wanahitajia misaada ya dharura ya chakula. 

Mark Lowcock amesema kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa wanajeshi wa Eritrea hawajaondoka katika eneo la Tigray.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amesty International pia limeripoti kuwa, jeshi la Eritrea lingali linaua raia katika eneo la Tigray, wiki chache baada ya Ethiopia kutangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo jirani yake wameanza kuondoka katika eneo hilo linalokumbwa na mgogoro na mapigano kwa miezi kadhaa sasa.

Tigray

Amnesty imesema mauaji ya Jumatatu ya wiki hii katika mji wa Adwa ni mfano hai wa mwendelezo wa ukatili unaofanywa na wanajeshi wa Eritrea dhidi ya raia wa Ethiopia katika eneo la Tigray.

Mwezi uliopita wa Machi shirika la Amesty International lilitangaza kuwa jeshi la Eritrea limefanya mauaji ya umati katika eneo hilo la Tigray. 

Tags