Apr 17, 2021 06:03 UTC
  • Maelfu waandamana dhidi ya serikali nchini Algeria

Maelfu ya watu wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya Algeria wakitaka kuachiwa huru wanaharakati wa kisiasa na kutoa wito wa kususiwa uchaguzi mkuu wa mapema wa Bunge nchini humo.

Waalgeria wameendelea kulalamikia hali mbaya na utendaji usiofaa wa serikali ya Abdelmadjid Tebboune licha ya kupita miaka miwili sasa tangu rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika alipong'atuka madarakani. 

Waandamanaji wa Algeria wanaamini kuwa, uchaguzi wa Disemba mwaka 2019 uliopelekea kushika madaraka Rais Abdelmadjid Tebboune umehuisha serikali ya zamani ya nchi hiyo na kuwarejesha madarakani viongozi wa serikali ya Bouteflika. 

Tarehe 18 mwezi Februari mwaka huu Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria alilivunja Bunge la nchi hiyo kutokana na maandamano makubwa na mtawalia ya wananchi na kutoa agizo la kufanyika uchaguzi mpya tarehe 12 Juni. 

Rais wa Algeria ametangaza kuwa, lengo la kuvunjwa Bunge ni kufanyika uchaguzi usio wa kifisadi utakalofungua milango kwa ajili ya vijana.    

Tags