Apr 17, 2021 07:57 UTC
  • John Pombe Magufuli
    John Pombe Magufuli

Baadhi ya viongozi walioshiriki katika kikao cha 75 cha mkutano wa 59 wa Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika jana Ijumaa mjini New York wamebainisha alama za uongozi za rais wa awamu ya tano wa Tanzania, John Magufuli wakishauri kuendelezwa mema aliyoyatenda na kuahidi kushirikiana na Rais wa sasa wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.

Kikao hicho kilichoongozwa na Volkan Bozkir ambaye ni Rais wa Baraza Kuu la UN kilikuwa na ajenda mbalimbali  ikiwemo ya kutambua mchango wa John Magufuli aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo Machi 17, 2021 jijini Dar es Salaam.

Akitaja baadhi ya maeneo ya kumuenzi Magufuli, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema atakumbukwa kwa mchango wake katika kurejesha maadili ya utumishi wa umma, kupambana na rushwa, ujenzi wa miundombinu na mapinduzi ya viwanda ambayo ni msingi katika ukuaji uchumi.

Guterres ameongeza kuwa: "Tanzania imefanikiwa kufikia nchi ya watu wenye kipato cha kati miaka minne kabla ya kufikia 2025, na Magufuli alifanikiwa kuwezesha mfumo wa elimu bila malipo iliyowezesha watoto wengi kuongezeka shuleni, pia alifanikiwa kusogeza huduma za umeme vijijini kwa jitihada za kufikia wananchi wengi."

John Pombe Magufuli

Antonio Guterres ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, na kuwa pamoja na raia wa Tanzania katika juhudi zao za maendeleo.

Mwakilishi kutoka Ulaya Magharibi, amesema katika kikao hicho cha Umoja wa Mataifa kwamba John Magufuli alikuwa kiongozi aliyejitoa kwa ajili ya kuwaletea Watanzania maendeleo na kwamba juhudi zake zilitambulika kwa kiwango kikubwa kupitia sekta ya elimu na miundombinu.

 Kifo cha Magufuli kilitokea saa 12.00 jioni, Machi 17, mwaka huu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam baada ya kusumbuliwa na maradhi ya moyo.

Tags