Apr 19, 2021 11:21 UTC
  • Mshauri wa Rais wa Algeria: Ufaransa ilieneza ujinga nchini zama za ukoloni

Mshauri wa Rais wa Algeria amesema kuwa Ufaransa ilifanya kazi ya kueneza ujinga wa kutojua kusoma na kuandika wakati wa ukoloni wa nchi hiyo nchini Algeria.

Matamshi hayo ya Abdelmajid Al-Sheikhi yametolewa huku uhusiano wa nchi hizo mbili ukikumbwa na mdororo mpya.

Mshauri wa Rais wa Algeria amesema kuwa, mwaka 1830 kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika nchini Algeria kilikuwa hakizidi asilimia 20 na kwamba, katika kipindi cha miaka ya ukoloni wake nchini humo, Ufaransa iliangamiza kizazi cha walimu katika operesheni iliyoandamana na uporaji mkubwa na kuchafua fikra za raia wa Algeria

Siku chache zilizopita pia Waziri wa Kazi wa Algeria, el Hachemi Djaaboub aliitaja Ufaransa kuwa ni adui wa jadi na wa siku zote za nchi hiyo, matamshi ambayo yamepingwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa. 

El Hachemi Djaaboub amesema kuwa, Algeria imeitaka Ufaransa iwalipe fidia wananchi wa nchi hiyo kutokana na kufanya majaribio ya nyuklia katika ardhi ya Algeria miaka 60 iliyopita na kuhatarisha usalama wa raia tangu wakati huo hadi hivi sasa.

Majaribio ya silaha za nyuklia ya Ufaransa nchini Algeria

Ufaransa iliikoloni na kuikalia kwa mabavu Algeria kwa miaka 132 na hatimaye nchi hiyo mwaka 1962 ikapata uhuru baada ya miaka mingi ya mapambano ya ukombozi ya umwagaji damu. Raia wa Algeria milioni moja waliuwa katika mapambano ya kuikomboa nchi yao dhidi ya Ufaransa. 

Tags