Apr 20, 2021 07:59 UTC
  • Usalama wa kikanda; ajenda ya mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Algeria na Libya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria jana Jumatatu alikutana na mwenzake wa Libya na kufanya mazungumzo kuhusu usalama wa kikanda na kuziunga mkono pande za Libya kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Sabri Boukadoum Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria na mwenzake wa Libya Najla al Mangoush wamejadili kuhusu hatari zinazotishia usalama wa eneo kama vile ugaidi, jinai zilizoratibiwa kutoka nje, biashara ya madawa ya kulevya, magendo ya silaha na wahamiaji haramu.  

Katika mazungumzo hayo Boukadoum ameeleza kuwa, Algeria itatekeleza juhudi zake zote ili kukuza kiwango cha uhusiano wa nchi mbili na kuziunga mkono pande za Libya ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa nchi hiyo. 

Algeria ambayo iko karibu na Libya na ikiwa na mpaka wa pamoja na nchi hiyo wa umbali wa kilomita elfu moja  ina wasiwasi na hali  ya ukosefu wa amani katika nchi jirani na inafanya kila iwezalo kuimarisha ushawishi wake katika uga wa diplomasia ya kikanda. 

Nchi jirani na Libya na Algeria kuimarisha zaidi uhusiano 

Libya ilikumbwa na mgogoro wa kisiasa na ukosefu wa amani tangu wananchi wa nchi hiyo walipofanya mapinduzi mwaka 2011 na kumuondoa madarakani dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kwa uingiliaji kati wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za kieneo.  

Tags