Apr 21, 2021 07:40 UTC
  • AU, UN na EU zalaani mauaji ya Rais Idriss Deby wa Chad

Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Ulaya (EU) zimelaani na kukosoa vikali mauaji ya Rais Idriss Deby Itno wa Chad.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Chad ameeleza kusikitishwa na mauaji hayo, huku akitoa mkono wa pole kwa familia ya Deby, serikali na taifa la Chad kwa ujumla kufuatia kifo cha kiongozi huyo.

Naye Volkan Bozkir, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema UN imesikitishwa mno na habari za mauaji ya Deby, na imetuma risala za rambirambi kwa familia ya Deby.

Sambamba na kunyoosha mkono wa pole, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema pande zote husika nchini Chad zinapaswa kuwa makini na kutanguliza mbele suala la uthabiti wa nchi hiyo na eneo la Sahel kwa ujumla. Kadhalika Charles Michel, Rais wa Baraza la EU amesisitiza kuwa, uthabiti, usalama na mamlaka ya kujitawala Chad zinapaswa kulindwa.

Mousa Faki Mahamat (kushoto) na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres

Hapo jana, Jeshi la la Taifa la Chad lilitangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa Idriss Deby ameaga dunia akipigana kwa ajila ya kulinda ardhi ya nchi hiyo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Deby ameuawa akipambana na magaidi waliotokea nchi jirani ya Libya huko Kaskazini mwa Chad alikokwenda kukagua jeshi la nchi hiyo linalopigana na makundi ya kigaidi.

Idriss Deby ambaye ameiongoza Chad kwa kipindi cha miaka 30, ameuawa kabla ya kuapishwa kuingoza nchi hiyo kwa awamu ya sita baada ya Kamisheni ya Uchaguzi kumtangaza mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 11 mwezi huu wa Aprili. Mwanawe Jenerali Muhammad Idriss Déby Itno anatazamiwa kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mpito cha miezi 18 kabla ya kuitishwa uchaguzi mwingine.

Tags