Apr 21, 2021 11:37 UTC
  • Baada ya mtoto wa Deby kuchukua uongozi wa Chad, EU yataka katiba iheshimiwe

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amezitaka pande husika nchini Chad kujizuia na kuheshimu katiba ya nchi hiyo baada ya Rais wa nchi kuuawa.

Josep Borrell amesema hayo katika taarifa yake rasmi akisisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unataka utulivu uwepo nchini Chad, katiba iheshimiwe na kuandaliwe mazingira ya kufanyika uchaguzi. 

Wito huo wa Umoja wa Ulaya unatolewa katika hali ambayo, nchini Chad tayari kumeundwa Baraza la Kijeshi linaloongozwa na mtoto wa kiume wa Rais Idriss Deby, Jenerali Muhammad Idriss Déby Itno (maarufu kama Mahamat Kaka) litakaloongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mpito cha miezi 18.

Baraza hilo limeundwa wakati ambapo kwa mujibu wa katiba ya Chad Spika wa Bunge ndiye anayepaswa kuchukua madaraka ya nchi iwapo Rais ataaga dunia au kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Idriss Deby  aliyekuwa Rais wa Chad

 

Idriss Deby aliaga dunia jana kutokana na majeraha aliyoyapata katika medani ya vita.

Deby aliuawa akipambana na magaidi waliotokea nchi jirani ya Libya huko kaskazini mwa Chad alikokwenda kukagua jeshi la nchi hiyo linalopigana na makundi ya kigaidi.

Idriss Deby ambaye ameiongoza Chad kwa kipindi cha miaka 30, ameuawa kabla ya kuapishwa kuingoza nchi hiyo kwa awamu ya sita baada ya Kamisheni ya Uchaguzi kumtangaza mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 11 mwezi huu wa Aprili.