Apr 23, 2021 02:32 UTC
  • AU: Tuko tayari kusimamia mazungumzo ya kukwamua mgogoro wa kisiasa Somalia

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limesema liko tayari kuandaa na kusimamia mazungumzo ya kukwamua mgogoro wa kisiasa unaoikabili Somalia.

Balozi Bankole Adeoye, Kamishna wa masuala ya siasa, amani na usalama wa Umoja wa Afrika amesema AU inaziasa pande zote husika za kisiasa nchini Somalia kulichukulia kwa uzito suala la kufanyika mazungumzo hayo jumuishi ya kisiasa, kwa lengo la kuliondoa taifa hilo la Pembe ya Afrika katika mkwamo wa kisiasa.

Tayari Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo amekaribisha pendekezo la AU kuwa mpatanishi wa mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa uchaguzi unaoikabili nchi yake.

Haya yanajiri wiki moja baada ya Farmaajo kutia saini sheria ya kuongeza muda wa kukaa madarakani kwa miaka miwili, baada ya Bunge la nchi hiyo kupasisha muswada wa sheria hiyo .Aprili 12, Wabunge nchini Somalia walipasisha muswada huo baada ya serikali ya Rais Farmajo kushindwa kuandaa uchaguzi mwezi Februari mwaka huu baada ya muda wake kumalizika.

Rais wa Somalia akifuatilia hotuba

Muda wa kukaa madarakani kwa Farmaajo ulikwisha tarehe 8 mwezi Februari huku bunge likiwa limemaliza muda wake tangu mwezi Desemba, huku uchaguzi wa wabunge na rais uliokuwa ukipaswa kufuata ukikumbwa na mizozo ya kisiasa.

Viongozi wa upinzani wa Somalia na wa majimbo ya Jubbaland na Puntland pamoja na baraza la seneti , walikataa uamuzi wa bunge na wamesisitiza kwamba, wataendelea kupinga uamuzi huo. Wafadhili wa Somalia, zikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya  zimetangaza kupinga uamuzi huo.

Tags