Apr 23, 2021 12:05 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Watu milioni 4.5 wanahitajia msaada wa chakula  Tigray, Ethiopia

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watu wasiopungua milioni 4.5 wanahitajia msaada wa chakula wa kuokoa maisha yao katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.

Hayo yameelezwa na Stéphane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa  ambaye amebainisha kwamba, umoja huo una wasiwasi wa kuongezeka zaidi idadi ya watu katika jimbo hilo wanaohitajia msaada wa chakula.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, jimbo la Tigray linahitaji misaada zaidi ili kuzuia kutokea maafa ya kibinadamu kutokana na hali mbaya ya ukosefu wa chakula na ukata wa huduma muhimu unaoshuhudiwa katika eneo hilo.

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha pia kuwa, tishio la usalama wa chakula limesababishwa na ukosefu wa usalama ulioshuhudiwa katika eneo hilo na kusababisha kusitishwa kikamilifu kilimo.

Hali ya wakimbizi katika jimbo la Tigray Ethiopia

 

Aidha amesema, hali bado si shwari huko Tigray na kwamba, kuendelea ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo kunakwamisha juhudi za ufikishaji misaada ya kibinadamu, 

Majuzi Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulitangaza kuwa, licha ya kupita miezi sita tangu kulipoibuka mgogoro wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia bado kungali kunaripotiwa taarifa za kufanyika vitendo vya unyanyasaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray.