Apr 24, 2021 13:00 UTC
  • Zanzibar kuanzisha Mfuko Maalum wa Zaka kwa ajili ya kuisaidia jamii

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inakaribia kukamilisha mpango wa kuanzisha Mfuko Maalum wa Zaka ambao utatumika kuwasaidia watu wenye mahitaji visiwani humo.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman alipokuwa akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Ijumaa katika msikiti wa Masjidu-Sahaabah, Mtoni, mjini Unguja.

Akiwahimiza waumini kuhusu umuhimu wa kutoa Zaka na sadaka, Othman amesema: "Mwenyezi Mungu anawasifia wale wanaotow miongoni mwa waja wake aliowaruzuku, lakini anaeleza kwamba hicho alichowaruzuku hakimaanishi kuwa ni chao. Bali wamepewa ili waweze kutoa. Na hakuna anayefilisika kwa sababu ya kutoa kwa wengine wenye uhitaji."

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema, uamuzi wa kuwa na Mfuko wa Zaka ulishapitishwa tangu mwaka 2007 na kwamba utekelezwaji wake utawezekana hivi karibuni.

Waumini wakisali Sala ya Idi

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema kuna matajiri wengine wa Kiislamu nje ya Zanzibar ambao wanataka sana kutowa Zaka zao kwa ndugu zao waliopo Zanzibar, lakini wamekosa chombo cha kuzikabidhisha Zaka hizo.

“Kwa kuwa na mfuko huu, hawa ndugu zetu walioko nje ya Zanzibar nao watakuwa na mahala wanapopaamini kuleta sadaka na Zaka zao wakijuwa kuwa zitatumika kwa malengo waliyoyakusudia,” aliongeza Mheshimiwa Othman.

Katika hatua nyengine, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kujitokeza bila woga kuwachangia ndugu zao wanaoendelea kushikiliwa katika magereza ya Tanzania Bara ambako wanakabiliwa na mashitaka ya ugaidi, maarufu kama Masheikh wa Uamsho.

Mheshimiwa Othman amesema, si kosa kisheria kwa mtu yeyote kuwachangia washukiwa hao, kwani mbali ya wenyewe kuwa mikononi mwa vyombo vya dola, bado wana haki zao na wanahitaji kuwalipia mawakili wanaowatetea pamoja na kuziendesha familia zao.../

 

 

 

 

 

Tags