Apr 28, 2021 08:00 UTC
  • UN: Kuna ongezeko la hatari kwa watoto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, amesema watoto 370,000 kwa sasa ni wakimbizi wa ndani nchini kote kwa sababu ya vurugu zinazoendelea na ukosefu wa usalama.

Fran Equiza amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva na kuongeza kuwa hicho ni kiwango cha juu kabisa cha watoto kufurushwa katika makazi yao tangu mwaka 2014.

Equiza amebainisha kwamba kwa makadirio ya hivi karibuni, takribani watoto 168,000 walilazimishwa kukimbia nyumbani kwao kutokana na vurugu zilizotapakaa, zikitokana na uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Desemba nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Afisa huyo wa UNICEF amesema, shirika hilo la UN linaonya juu ya hatari zinazozidi kuongezeka kwa watoto, pamoja na kuathiriwa na unyanyasaji wa kingono na mwili, kuajiriwa katika vikosi vya jeshi na makundi ya wapiganaji, kuongezeka kwa viwango vya utapiamlo na ufikiaji mdogo wa huduma muhimu.

Aidha ameongeza kuwa asilimia 53 ya idadi ya watu nchini humo, ambao nusu yao ni watoto, wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Inafaa kuashiria kuwa, licha ya changamoto kubwa, pamoja na mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu, UNICEF inaendelea kuimarisha shughuli zake za ulinzi wa watoto kote nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jitihada hizo ni pamoja na kupelekwa kwa timu za ulinzi wa watoto ambazo zinaweza kufikia watoto walio katika mazingira magumu.../

Tags