May 07, 2021 02:24 UTC
  • 'Maulamaa wa Algeria waendeshe Jihadi ili kutokomeza mabaki ya utamaduni wa Kifaransa'

Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Algeria lillo chini ya ofisi ya rais wa nchi hiyo amesema, Maulamaa wa Kiislamu wa nchi hiyo inapasa waendeleze jihadi ya kielimu na kitaifa kwa ajili ya kung'oa na kutokomeza mabaki ya utamaduni wa Kifaransa.

Abu Abdullah Ghulamullah ameyasema hayo katika hafla iliyoandaliwa na jumuiya ya maulamaa wa Kiislamu wa Algeria kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 90 tangu kuasisiwa kwa jumuiya hiyo, ambapo pamoja na mambo mengine amepongeza mchango wa maulamaa wa Algeria katika kupambana na njama za kufuta utambulisho wa nchi hiyo zilizoendeshwa katika kipindi cha ukoloni wa Ufaransa kuanzia 1830 hadi 1962.

Ghulamullah ameeleza kuwa, Algeria inawahataji watoto wake ambao wanapambana kwa ajili yake na wanaipenda ili kuhakikisha nchi hiyo inajitoa kwenye makucha ya ukoloni unaotaka kuidhibiti na ambao ungali unaendelea kuitwisha utamaduni wake.

Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Algeria ameongeza kuwa, Maulamaa wa Kiislamu wa Algeria inapasa waendeleze jihadi ya kielimu na kitaifa kwa ajili ya kung'oa na kutokomeza mabaki ya utamaduni wa Kifaransa.

Wataalamu na wanahistoria wanasema, sababu ya kuenea Kifaransa nchini Algeria ni kufanywa lugha hiyo jambo la lazima wakati wa enzi za ukoloni na kampeni iliyoendeshwa ya kupiga vita lugha ya Kiarabu na vile vile kucheleweshwa utekelezaji wa sheria ya utumikaji wa lugha hiyo ya taifa katika shughuli za kiserikali na mfumo wa elimu wa nchi hiyo.

Algeria ni moja ya nchi zinazotumia zaidi lugha ya Kifaransa; kiasi kwamba, kwa mujibu wa jumuiya ya usimamizi wa Kifaransa iliyo chini ya shirika la kimataifa la Francophone, watu zaidi ya milioni 275 wanazungumza lugha ya Kifaransa duniani kote, ambao miongoni mwao ni Waalgeria milioni 13 na laki nane, ikiwa ni theluthi moja ya karibu watu wote milioni 43 wa nchi hiyo.../

Tags