May 07, 2021 07:59 UTC
  • Tanzania yaonya kuhusu Corona ya India, spishi hiyo yaripotiwa Kenya na Uganda

Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimetadharisha juu ya kuibuka na kuenea kwa spishi mpya ya ugonjwa wa Covid-19 ya India katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wakati Serikali ya nchi hiyo ikiimarisha ukaguzi, upimaji na ulinzi dhidi ya virusi vya Corona katika viwanja vya ndege na mipakani, wataalamu wa afya wametoa angalizo kuhusu tabia ya virusi vipya vilivyoibuka nchini India.

 Mjadala kuhusu uwezekano wa kurejea upya kwa maambukizo ya virusi vya corona umeanza kujitokeza, hasa kutokana na uhusiano wa karibu baina ya Watanzania wenye asili ya India ambao huenda nchini humo na kurejea nchini mara kwa mara.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akitoa angalizo kwa Serikali kuhusu virusi hivyo. Amesema kuna watu kipimo kinaweza kuonyesha hawana maambukizo wakati wana dalili zote za corona na kwamba India watu wameugua hata kupoteza maisha lakini vipimo vilionyesha hawakuwa na maambukizo.

Miili ya walioafariki kwa Corona India ikiteketezwa

Amesema, “Hili ni angalizo muhimu sana kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kama inavyoshauriwa, vaa barakoa, epuka mikusanyiko kadri uwezavyo, hali siyo salama. Tusubiri ripoti ya tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili tujue mwelekeo wa nchi juu ya njia nyingine za kujikinga."

Jana Serikali ya Tanzania ilisitisha safari za ndege zote kutoka India kuingia nchini na kuzuia zile zinazofanya safari za huko, kufuatia aina mpya ya virusi vya Covid-19 inayoongeza maambukizo na vifo nchini humo.

Haya yanajiri huku kesi kadhaa za spishi hiyo hatari ya Corona zikiripotiwa katika nchi jirani za Kenya na Uganda.

Tags