May 10, 2021 12:36 UTC
  • Waasi wa kundi la FACT waliotekwa nyara na jeshi la Chad
    Waasi wa kundi la FACT waliotekwa nyara na jeshi la Chad

Jeshi la Chad limejitangazia ushindi dhidi ya waasi kufuatia mapigano ya wiki kadhaa yaliyosababisha kifo cha Rais wa muda mrefu wa nchi hiyo, Idriss Deby kwenye uwanja wa vita.

Mkuu wa Jeshi la Chad Jenerali Abakar Abdelkerim Daoud amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Kurejea jeshi kambini kwa ushindi ni ishara ya kumalizika operesheni ya vita na ushindi wa Chad."

Jenerali Abdelkerim Daoud amesema kuwa, jeshi limefanikiwa kumaliza vita na kurejesha usalama na sasa linadhibiti ardhi yote ya Chad.
Jeshi la Chad limedai kuwa limeua mamia ya waasi.

Katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena, umati wa watu ulionekana ukishangilia jana jioni wakati wanajeshi walipokuwa wakirudi kutoka mstari wa mbele wa vita wakiwa kwenye safu ndefu ya mizinga na magari ya kivita.

Hata hivyo taarifa iliyotolewa na kundi la waasi la Front for Change and Concord in Chad (FACT) imesema kwamba, kundi hilo halina habari yoyote kuhusu kumaliza mapigano.
Wakati wa uchaguzi wa rais wa Chad tarehe 11 Aprili, waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo walianzisha mashambulio makali karibu na maeneo ya mpakani wakitaka kukomeshwa utawala wa miaka 30 wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Idriss Deby.

Idriss Deby

Kiongozi huyo alitembelea wanajeshi kwenye uwanja wa vita siku moja baada ya kudai kwamba, ameshinda tena uchaguzi wa rais na akajeruhiwa katika shambulio lililosababisha kifo chake. Mauaji ya Idriss Deby yameitumbukiza zaidi nchi hiyo masikini kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa.

Baraza la kijeshi, ambalo linaongozwa na mtoto wa Deby, Mahamat Idriss Itno, 37, lilichukua madaraka ya nchi mara tu baada ya mauaji ya Deby.
Mahamat Idriss Itno ametangaza serikali ya mpito itakayoiongoza Chad kwa miezi 18 na kuitisha uchaguzi huru.

Tags