May 11, 2021 07:42 UTC
  • FAO: Hali ya kilimo barani Afrika ni mahututi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, amesema kuwa, kilimo kinaadhibiwa vibaya barani Afrika na hali ya sekta hiyo muhimu na ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa dunia, ni mahutudi barani humo.

QU Dongyu, amesema hayo mjini Rome Italia wakati wa uzinduzi wa ripoti ya FAO, iitwayo ‘Matumizi ya Umma juu ya Chakula na Kilimo katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara Barani Afrika,’ ambayo inaonesha pengo kubwa kati ya ahadi za kisiasa za muda mrefu na ukweli wa kifedha katika nchi 13 za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Amebainisha kuwa ripoti hiyo inatokana na "uchambuzi wa kina zaidi ya miaka 15 iliyopita, uliowezekana kutokana na ushirikiano mkubwa na wanachama wa FAO katika ukanda huo." 

Umoja wa Mataifa unalalamika kwamba, ingawa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa dunia, lakini sekta hiyo imetupwa barani Afrika

 

FAO inakumbusha kuwa mkutano uliofanyika mjini Maputo Msumbiji mnamo mwaka 2003 na kufanyika tena mjini  Malabo, Equatorial Guinea, mwaka 2014, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ziliahidi kutoa asilimia 10 ya bajeti zao za kitaifa kwa chakula na kilimo, katika juhudi za kukuza ukuaji wa kijamii na kiuchumi, hata hivyo karibu miongo miwili na kuendelea imepita lakini ahadi hiyo bado haijatimizwa. 

Kati ya nchi zilizofanyiwa utafiti na mpango wa Ufuatiliaji na Uchambuzi wa Sera ya Chakula na Kilimo, MAFAP ambao ni mpango wa FAO, ni nchi moja tu, Malawi, ndiyo iliyotimiza lengo la kwa asilimia 10; nyingine ni Mali, ambayo ilifikia kwa miaka kadhaa kiwango hicho. Amma nchi 11 zilizobaki ambazo Benin, Burkina Faso, Burundi, Ethiopia, Ghana, Kenya, Msumbiji, Rwanda, Senegal, Tanzania na Uganda hazijafanikiwa kufanya hivyo.