May 11, 2021 07:47 UTC
  • Watu 6 wauawa katika mripuko wa kigaidi mjini Mogadishu, Somalia

Polisi nchini Somalia wametangaza habari ya kuuawa maafisa 6 wa polisi baada ya gaidi mmoja kujiripua kwa bomu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, polisi wa Somalia wametangaza kuwa, mripuko huo umetokea mbele ya kituo cha polisi mjini Mogadishu na kuua maafisa 6 wa polisi na kujeruhi wengine 6.

Genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab limetangaza kuhusika na mripuko huo.

Mashambulizi ya kigaidi yameongezeka nchini Somalia na katika mji mkuu wa nchi hiyo kiasi kwamba, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa, zaidi ya watu 250,000 wamekimbia makazi yao katika kipindi cha wiki mbili tu zilizopita kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mara kwa mara genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab hutangaza kuhusika na mashambulio Somalia

 

Huku maeneo yaliyoshuhudia wimbi hilo la wakimbizi yakiwa ni Banadir, Berdale na Badweyn, lakini mji wa Mogadishu nao umeshuhudia watu wengi wakikimbia makazi yao.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa aidha imesema, machafuko yamesababisha pia ukosefu wa utulivu na kuvuruga kazi za misaada ya kibinadamu. Kuwafikia walengwa imekuwa ni tabu sana kutokana na changamoto za kiusalama katika mji wa Mogadishu, huku baadhi ya maeneo ya Somalia yakiwa hayafikiki kabisa.

Wakimbizi 14,000 waliokimbilia katika maeneo 26 ya wilaya za Garasbaly na Kahda wameshindwa kupatiwa msaada wowote hadi hivi sasa. OCHA imesema, watu hao wanahitajia mno misaada ya chakula, makazi, mahitaji yasiyo ya chakula, ulinzi na misaada ya afya.

Tags