May 11, 2021 12:13 UTC
  • Shekhe Mkuu wa Al Azhar: Kimya cha dunia mbele ya ugaidi wa Wayazuni kinatia aibu

Shekhe Mkuu wa Al Azhar amelaani kimya kinachoonyeshwa na walimwengu mbele ugaidi wa kinyama wa Wazayuni na hujuma wanazofanya dhidi ya msikiti wa Al Aqsa na Wapalestina.

Shekhe Mkuu wa Al Azhar ya Misri, Ahmed el-Tayeb amesema, kimya kinachoonyeshwa na walimwengu mbele ya ugaidi wa kinyama wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina wakazi wa Quds tukufu na dhidi ya msikiti mtukufu wa Al Aqsa kinatia aibu.

Shekhe Ahmed el-Tayeb amewatumia salamu za maamkizi ya amani wananchi wa taifa madhulumu la Palestina na akasisitiza kwamba, "kadiri muda unavyopita, ndivyo Palestina itakavyoendelea kusimama imara kukabiliana na mataghuti na haitasalimu amri; na wananchi wa Palestina wataendelea kutetea na kulinda ardhi yao, maharimu zao pamoja na matukufu yao, ukiwemo msikiti wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu."

Hujuma za askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika msikiti wa Al Aqsa

Kwa muda wa siku kadhaa sasa msikiti wa Al Aqsa na maeneo yaliyouzunguka katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) yanashuhudia hujuma na mashambulio makali ya askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel waliodhamiria kutekeleza njama ya utawala huo ghasibu ya kuiyahudisha Quds na kuugawanya msikiti wa Al Aqsa kieneo na kiwakati katika utumiajiwake. Mamia ya Wapalestina wakazi wa mji huo wa Baitul Muqaddas wamejeruhiwa hadi sasa kutokana na muqawama walioonyesha kukabiliana na njama hiyo.../