May 13, 2021 13:32 UTC
  • Serikali ya Mpito  ya Chad yapasisha mpango wa kisiasa

Serikali ya Mpito ya Chad imepasisha mpango wake wa kisiasa wakati wa kikao cha dharura cha baraza la mawaziri. Rasimu ya mpango huo itawasilishwa Ijumaa ya kesho katika Bunge la nchi hiyo lililofutwa baada ya kifo cha rais Idriss Deby Itno.

Ilichukua dakika thelathini tu kwa serikali, iliyokutana katika kikao kilichoongozwa na kiongozi wa mpito, Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno, kupasisha mpango wa kisiasa wa serikali ya Waziri Mkuu Albert Pahimi Padacké aliyeteuliwa Mei 2. Mpango huo unaonyesha "mwendelezo wa shughuli za Serikali, utunzaji wa amani na utulivu na kuendelea na mipango na miradi ya maendeleo" hadi mwezi Oktoba 2023.

Mnamo Mei 14, wabunge wa Bunge la zamani, walirejeshwa tena ili kuidhinisha mpango wa kisiasa wa serikali ya Waziri Mkuu Albert Pahimi Padacké.

Wakati huo huo, wanasiasa mbalimbali na mashirika ya kiraia yanaendela na msimamo wa kuandamana dhidi ya baraza la kijeshi la mpito, ambalo wanasema bado liko mamlakani kinyume na katiba.

Mahamat Idriss Deby, Kiongozi wa Baraza la Kijeshi la Chad

 

Ikumbukwe kuwa, Baraza la Kijeshi la Chad linaloongozwa na mtoto wa Deby, Mahamat Idriss Deby, lilichukua madaraka ya nchi baada ya kiongozi huyo kuuawa na kuahidi kufanya uchaguzi ndani ya miezi 18.

Hata hivyo hatua hiyo inalalamikiwa na wananchi wa Chad ambao wamekuwa wakipinga jeshi kuchukua hatamu za nchi.

Watu kadhaa wameshauawa nchini Chad katika ukandamizaji wa jeshi dhidi ya waandamanaji wanaotaka demokrasia ichukue mkondo wake.

Idris Deby ambaye alikuwa ameiongoza Chad kwa kipindi cha miaka 30, aliuawa hivi karibuni kabla ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita baada ya Kamisheni ya Uchaguzi kumtangaza mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili.