May 13, 2021 13:33 UTC
  • Mjukuu wa Mandela atoa wito wa kufungwa ubalozi wa Israel nchini Afrika Kusini

Maelfu ya raia wa Afrika Kusini vikiwemo vyama na baadhi ya watu muhimu na mashuhuri wamefanya maandamano na kukusanyika katika maeneo mbalimbali muhimu kama mbele ya Bunge na kutoa wito wa kususiwa utawala haramu wa Israel.

Miji muhimu ya Afrika Kusini jana ilishuhudia maandamano na mikusanyiko ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina ambapo waandamanaji walitangaza pia chuki na upinzani wao wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Waandamanaji mjini Cape Town walifanya maandamano na kuelekea upande wa jengo la Bunge nchini humo huku wakipiga nara za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina. Mjukuu wa shujaa wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mandla Mandela aliyeshiriki katika maandamano hayo ametoa wito wa kufungwa ubalozi wa utawala haramu wa Israel nchini humo.

Maandamano ya wananchi wa Afrika Kusini ya kuunga mkono wananchi wa Palestina

 

Mjukuu huyo wa Mandela amesema, licha ya Israel kuwauwa kinyama watoto wa Kipalestina lakini ulimwengu umeendelea kunyamaza kimya. Aidha amesema, wakati linapozungumziwa suala la Palestina, sisi tukiwa Waafrika Kusini tuna umoja na tunapaza sauti moja kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Siku ya Jumanne pia, watu wasiopungua 300 walikusanyika mbele ya ubalozi wa utawala dhalimu wa Israel nchini Afrika Kusini na kutoa wito wa kususiwa utawala huo ghasibu unaoendelea kutenda mauaji kila uchao dhidi ya Wapalestina kwa uungaji mkono wa Marekani na madola ya Magharibi.