May 14, 2021 11:46 UTC
  • Mahakama Kuu ya Kenya yapinga mpango wa BBI wa kubadili katiba

Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamua kwamba, mageuzi ya kikatiba yanayopigiwa debe na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga ni kinyume na sheria.

Wakosoaji wanasema mpango huo ilibuniwa kumzuia na kumfutilia mbali Naibu Rais William Ruto, ambaye amepingana hadharani na Rais Uhuru kenyatta.

Kwenye uamuzi wake wa Alhamisi (Mei 13), mahakama hiyo ilisema rasimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba, maarufu kama Building Bridge Initiatives (BBI), ni hatua binafsi ya Rais Kenyatta ambaye hana mamlaka ya kisheria kuanzisha mchakato wa mabadiliko yoyote ya kikatiba kupitia uhamasishaji wa umma.

Mpango huo ambao umeligawa taifa hilo la Afrika Mashariki kisiasa, unapendekeza kuuondoa mfumo wa mshindi wa uchaguzi kuchukua kila kitu, jambo ambalo Rais Kenyatta anasema limechochea migogoro ya kikabila ya baada ya uchaguzi.

Bunge la Kenya tayari lilipitisha marekebisho yaliyopendekezwa katika mpango wa BBI  ambayo yanaashiria mabadiliko makubwa kwa muundo wa serikali ya taifa hilo tangu katiba mpya ilipopitishwa mnamo 2010.

Mmoja wa majaji katika mahakama hiyo amesema: "Rais hawezi kuwa mchezaji na mwamuzi katika mechi moja."

Serikali ya Kenya, ambayo inataka kuitishwa kura ya maoni ya katiba mpya baada ya Kenyatta kutia saini muswada huo kuwa sheria, ilisema itakata rufaa kupinga uamuzi huo.

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta anasema muswada huo unaruhusu kugawana madaraka kati ya makabila yanayopinga ili kupunguza ghasia za uchaguzi. 

Mpango wa BBI pia utaunda majimbo mapya 70 ya uchaguzi, kurejesha jukumu la mawaziri wa serikali kwa wabunge waliochaguliwa, na kuunda nyadhifa kadhaa mpya zenye nguvu kama waziri mkuu, manaibu wawili wa rais na kiongozi rasmi wa upinzani wa bungeni.

Tags