May 14, 2021 11:47 UTC
  • Amnesty International: Wazungu na mbwa waliokolewa kabla ya watu weusi huko Palma, Msumbiji

Kundi la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema katika ripoti yake kwamba, wakandarasi wazungu walisafirishwa kwa ndege na kupelekwa maeneo yenye usalama kabla ya wenzao weusi baada ya shambulio la magaidi mwezi Machi mwaka huu katika mji Palma nchini Msumbiji.

Amnesty imesema, operesheni ya kuokoa watu katika shambulizi la kundi la kigaidi la al Shabab katika mji wa pwani wa Palma ilifanyika kwa ubaguzi kwa kuwaokoa kwanza wazungu na mbwa wao kabla ya watu weusi.

Katika ripoti hiyo iliyotayarishwa kutoka kwenye mahojiano na manusura 11 weusi, Amnesty imelalamika kwamba, hata mbwa waliokolewa kutoka kwenye hoteli waliyokuwa wamekimbilia na kupelekwa maeneo salama kwa kutumia helikopta kabla ya watu weusi. 
"Makandarasi wazungu walisafirishwa na kupelekwa eneo salama kabla ya watu weusi, na msimamizi wa hoteli aliwachukua mbwa wake wawili kwenye helikopta ya uokoaji, na kuwaacha nyuma watu weusi", imesema ripoti ya Amnesty International.

Watu 200, wengi wao wakiwa wafanyikazi na wageni wanaofanya kazi kwenye mradi wa gesi, walikimbilia hifadhi katika Hoteli ya Amarula Palma wakati wa shambulio la al Shabab Machi mwaka huu.

Amnesty inasema makandarasi wazungu walipewa kipaumbele zaidi katika operesheni ya uokoaji iliyowaacha nyuma watu weusi na kwamba, Waafrika walioachwa nyuma walijaribu kukimbilia hifadhi kwa njia ya nchi kavu lakini walishambuliwa na wapiganaji wa al Shabab.

Deprose Muchena, Mkurugenzi wa Amnesty International eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema: "madai haya ya kutisha ni ishara kwamba, mpango wa uokoaji ulifanyika kwa misingi ya ubaguzi wa rangi."

Muchena amesema kuwa, kuwaacha nyuma watu wakati wa shambulio la silaha kwa sababu tu ya rangi ya ngozi yao ni ubaguzi wa rangi.
Ameongeza kuwa, kitendo cha meneja wa hoteli cha kuchagua kuokoa mbwa wake badala ya watu weusi kinashtua na kutisha sana.

Palma, Msumbiji

Mji wa Palma ulio karibu na mradi mkubwa ya gesi wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 60 ulilengwa kwa mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha tarehe 24 mwezi Machi mwaka huu. 

Makumi ya raia waliuawa na wengine wasiopungua 11,000 walikimbia makazi yao baada ya wanamgambo hao kuuvamia mji huo huo.

Tarehe 5 Aprili Jeshi la Msumbiji lilitangaza kuwa limeukomboa kikamilifu mji wa Palma ulioko katika mpaka wa Msumbiji na Tanzania.

Tags