May 15, 2021 07:03 UTC
  • Maafa makubwa ya kibinadamu yanalijongelea eneo la Tigray, Ethiopia

Umoja wa Ulaya umelaani msimamo wa serikali ya Ethiopia wa kuendelea kufunga njia za kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo lililoharibiwa na vita la Tigray, la kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la AFP limemnukuu Janez Lenarčič, kamishna wa Umoja wa Ulaya wa kusimamia migogoro akisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, kutumia misaada ya kibinada kama silaha ya kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watu ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Vile vile amewaonya wanaohusika moja kwa moja na ukwamishaji huo kwamba watakuwa na kesi za kujibu kutokana na hatua zao hizo.

Tamko hilo la Umoja wa Ulaya limeongeza kuwa, watu wasiopungua milioni 5 na laki mbili kati ya jamii ya watu milioni 5 na laki saba wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia, wanahitajia misaada ya haraka ya chakula.

Wahanga wakuu wa hali mbaya ya Tigray Ethiopia na wanawake na watoto wadogo

 

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa tangu tarehe 3 Mei, ni asilimia 12 tu ya misaada ndiyo iliyowafikia watu milioni 3 wanaohitajia misaada ya haraka zaidi kama sehemu za kujisitiri na bidhaa nyingine zisizo za chakula.

Mwezi Disemba mwaka jana, Umoja wa Ulaya uliahidi kutoa msaada wa Euro milioni 90 kwa ajili ya wakazi wa Tigray, lakini ahadi hizo hazijatimizwa.

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray baada ya wakuu wa eneo hilo kuiasi serikali.

Maelfu ya watu waliuawa na zaidi ya laki 9 na 50 elfu walikimbia maeneo yao kutokana na mapigano hayo. Watu wasiopungua 50 elfu walikimbilia katika nchi jirani ya Sudan.

Tags