May 15, 2021 13:47 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Wapiganaji wa kigeni wangaliko Libya, ni ukiukaji wa usitishaji vita

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, wapiganaji wa kigeni na mamluki wangali wako nchini Libya, ukiwa ni ukiukaji wa mapatano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwaka jana; na akatoa mwito waondolewe nchini humo na kukomeshwa pia ukiukaji wa vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Katika ripoti aliyowasilisha Ijumaa kwa Baraza la Usalama la UN, Guterres amesema, makabidhiano ya madaraka yaliyofanyika mwezi Machi kwa njia ya amani kwa serikali mpya ya mpito umoja wa kitaifa (GNU) yamefufua matumaini mapya ya kuiunganisha tena Libya na taasisi zake na kwa ajili ya kupatikana amani ya kudumu. Hata hivyo amekumbusha kuwa, hatua inapasa zipigwe katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kiusalama ili kuwezesha chaguzi kufanyika kama zilivyopangwa mwishoni mwa mwaka huu.

Katika ripoti yake hiyo mpya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, serikali ya umoja wa kitaifa inapaswa kulipa kipaumbele suala la mageuzi katika sekta ya usalama, ikiwemo kujaza nafasi za juu za uteuzi wa maafisa wa kiraia na kijeshi, kuwasilisha ramani ya njia ya kuliunganisha upya jeshi la Libya na kushughulikia tatizo la utitiri wa makundi ya wabeba silaha.

Makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha, Libya

Makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa Oktoba 2020 baina ya pande hasimu nchini Libya yaliyoagiza pamoja na mambo mengine wapiganaji wote wa kigeni na mamluki waondoke katika ardhi ya Libya ndani ya muda wa siku 90, yalifungua njia ya kusainiwa mwafaka wa kuunda serikali mpya ya mpito ya umoja wa kitaifa na kuitishwa uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika Desemba 24 mwaka huu.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa hadi Desemba 2020 kulikuwepo na wapiganaji wa kigeni na mamluki wasiopungua 20,000 nchini Libya, wakiwemo Wasyria, Warussia, Wasudan na Wachad.

Mwezi uliopita wa Aprili, Baraza la Usalama la UN lilipitisha azimio lililohimiza vikosi vyote vya kigeni pamoja wapiganaji mamluki waondoke nchini Libya na kuidhinisha kutumwa nchini humo timu ndogo ya kusimamia makubaliano ya usitishaji vita.../

Tags