May 15, 2021 14:13 UTC
  • BAKWATA na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zaungana kimsimamo kuhusu Mashekhe wanaosota magerezani

Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda, ameungana na Baraza Kuu la Waislamu nchini humo BAKWATA kutaka kesi zinazowakabili mashekhe ziendeshwe haraka.

Shekhe Ponda ametoa wito huo kupitia waraka wa Idul-Fitri alioutoa kwa umma wa Watanzania.

Katika waraka huo, Shekhe Ponda ameishauri serikali ipeleke ushahidi mahakamani ili mashekhe hao na watuhumiwa wengine ambao kesi zao zimechukua muda mrefu, zitolewe hukumu.

“Tunaishauri serikali ipeleke ushahidi mahakamani ili mamia ya Waislamu wakiwemo mashekhe, maimamu, walimu wa madrasa, wasomi wa vyuo vikuu na waumini wa kawaida, inaowashikilia kwa tuhuma za ugaidi wapate haki ya kujitetea na kusomewa hukumu,” umesema waraka wa Shekhe Ponda.

Shekhe Ponda amesema, “tunaikumbusha serikali kuwa, ni kinyume na haki za binadamu kuwaweka watu gerezani na kuwatenga na shughuli zao na familia zao kwa miaka kadhaa, kwa madai ya kutafuta ushahidi.”

Mashekhe wa Uamsho Zanzibar ni miongoni mwa Waislamu wanaosota magerezani kwa miaka kadhaa sasa bila kesi zao kupatiwa ufumbuzi

Wito wa Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania unaenda sambamba na wito uliotolewa jana na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Nuhu Jabir Mruma, katika Baraza la Idul-Fitri, lililofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, ambapo Rasi Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.

Katika Baraza hilo, Mruma aliiomba serikali na vyombo vya utoaji haki, vishughulikie kwa haraka kesi za muda mrefu zikiwemo za Mashekhe walioko mahabusu na gerezani wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali.../

 

 

Tags