May 15, 2021 14:25 UTC
  • 30 wahukumiwa kifo Congo DR kwa kuhusika na ghasia za siku ya Idul Fitri

Watu thelathini wamehukumiwa kifo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kesi isiyosikilizwa katika siku moja tu, kwa kupatikana na hatia ya kuhusika na ghasia dhidi ya polisi wakati wa ibada ya Swala ya Idul Fitri ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Polisi mmoja aliuawa huko Kinshasa siku ya Alkhamisi wakati vikundi wili hasimu vya Waislamu vilipokuwa vikigombana juu ya kundi lipi linastahiki kuongoza ibada hiyo katika uwanja mkubwa wa michezo wa Kinshasa.

Wakili Chief Tshipamba amesema watu 30 wamehukumiwa kifo katika kesi iliyoanza Ijumaa, siku moja baada ya vurugu hizo.

Serikali ya mkoa wa Kinshasa imetangaza kuwa, mbali na mauaji ya afisa huyo wa polisi, watu wengine kadhaa walijeruhiwa, na gari moja la polisi liliteketezwa katika mapigano yaliyotokea nje ya Uwanja wa Mashahidi mjini Kinshasa.

Vikundi viwili vinavyopingana vimekuwa vikizozana kwa miaka mingi juu ya uongozi wa Jumuiya ya Waislamu ya Congo (Comico).

Jiji la Kinshasa lililoko Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kawaida hugubikwa na sherehe kubwa za kuadhimisha sikukuu ya Idul Fitri baada ya kukamilika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Sherehe hizo hufanyika katika viwanja vya umma na kwenye barabara kuu.

Waislamu wa Kinshasa kabla ya ghasia za Alkhamisi iliyopita katika Swala ya Idi

DRC haijatekeleza adhabu ya kifo tangu ilipositishwa mnamo 2003. Tangu wakati huo, hukumu za kifo zimebadilishwa kuwa kifungo cha maisha.

Tags