Jun 02, 2021 11:32 UTC
  • Familia za wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria zaitaka serikali kuwakomboa

Familia za wanafunzi waliotekwa nyara na magenge ya wahalifu nchini Nigeria na vilevile jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zimeitaka serikali ya Nigeria kuchukua hatua madhubuti za kukomboa karibu wanafunzi 200 wa shule moja ya Kiislamu waliotekwa nyara na magenge ya wahalifu katikati mwa Nigeria.

Tukio la karibuni zaidi katika mkondo huo ni lile la kutekwa nyara wanafunzi wasiopungua 136 siku ya Jumapili iliyopita katika Shule ya Kiislamu ya Salihu Tanko katika mji wa Tegina.
Wazazi wa wanafunzi hao wanaoendelea kusibiri nje ya shule hiyo wamesema wanaitaka serikali ya Abuja ifanye juhudi kubwa zaidi za kuwakomboa watoto wao na kuzuia kukariri uhalifu huo. 

Vilevile shirika la kutetea haki za binadamu la Save the Children limeihimiza serikali ya Nigeria kuchukua hatua zaidi za kuzuia utekaji nyara wa watoto.
Taarifa iliyotolewa na Save the Children imesema: "Ukosefu wa usalama na mashambulio dhidi ya shule vimezidisha idadi ya watoto wanaoshindwa kwenda kusoma mashuleni hasa katika sehemu ya Kaskazini mwa Nigeria". 

Shirika hilo limeitaka serikali na vyombo vya usalama vya Nigeria kufanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha watoto wanalindwa kutokana na mashambulizi ya magenge ya wahalifu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumatatu ya msemaji wa polisi ya Nigeria, Wasiu Abiodun, wanafunzi karibu 200 wa shule ya Kiislamu ya Salihu Tanko eneo la Rafi katika jimbo Niger walitekwa nyara na watu ambao walikuwa wakifyatua risasi kiholela. Katika tukio hilo mtu mmoja aliuawa.

Baadhi ya wanafunzi waliokombolewa wa Nigeria

Takwimu zinaonesha kuwa, tangu Disemba 2020 hadi sasa zaidi ya wanafunzi 700 wametekwa nyara na magaidi nchini Nigeria. Baadhi wameachiliwa huru baada ya vikomboleo kulipwa na wengine wameokolewa katika oparesheni za maafisa wa usalama.

Tags