Jun 05, 2021 02:31 UTC
  • Bobi Wine: Jamii ya kimataifa inathamini zaidi biashara kuliko maadili, haki za binadamu

Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi Sentamu maarufu kwa jina la Bobi Wine amesema hali ya haki za binadamu nchini Uganda imekuwa mbaya zaidi tangu baada ya uchaguzi wa Januari 14 mwaka huu.

Bobi Wine amesema Yoweri Museveni si rais halali wa Uganda na kwamba kuapishwa kwake kulifanyika kinyume cha sheria. Amesema atatumia kila fursa na kila nafasi za kidini au kitamaduni kuendeleza mapambano kwa ajili ya Uganda huru na ya kidemokrasia.

Amesema watu wa Uganda wanahisi kusalitiwa kwa kiasi kikubwa na jamii ya kimataifa na kwamba Jenerali Museveni anafadhiliwa na Wamagharibi.

Kiongozi wa upinzani wa Uganda amesema: "Vyombo vya habari vya kimataifa vinaripoti mauaji ya kiholela yanayofanywa na polisi na jinsi jeshi linavyotumiwa kukandamiza na kuua watu, lakini bado nchi za Magharibi zinaendelea kulifadhili jeshi hilo."

Bobi Wine

Robert Kyagulanyi amesema kuwa hali hiyo inawafanya waamini kuwa, jamii ya kimataifa inajali zaidi biashara na sio maadili na masuala kama demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria. Amezitaja nchi za Magharibi kuwa ni washirika katika uhalifu na waungaji mkono wa ugaidi wa ndani ambao amedai unafanywa na utawala wa Museveni.

Kiongozi wa siku nyingi wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni mwezi Mei mwaka huu alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliozusha utata na baadaye aliapishwa kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine.

Tags