Jun 08, 2021 15:53 UTC
  • Kushadidi harakati za ugaidi eneo la Afrika Magharibi

Katika wiki za hivi karibuni kumeshuhudiwa kushadidi Harakati za makundi ya kigaidi katika eneo la Afrika Magharibi hasa Nigeria na nchi jirani. Katika hatua ya hivi kairbuni kabisa magaidi walishambulia kijiji kaskazini mwa Burkina Faso na kuua raia zaidi ya 160 huku wakitetekteza nyumba na masoko. Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kulaani hujuma hiyo ambayo imepelekea idadi kubwa ya raia kuuawa kwa umati.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amebainisha wasiwasi wake kuhusu ugaidi huo na ametaka jamii ya kimataifa iimarishe jitihada za kukabiliana na hali hiyo hasa kuziunga mkono serikali za Afrika katika vita dhidi ya ugaidi.

Nchi mbali mbali za Afrika zimekuwa zikikabiliana na magaidi wakufurishaji na wanamgambao hasa kundi la kigaidi la Boko Haram lenye makao yake Nigeria na ambalo limeeneza ugaidi katika nchi jirani na pia kundi la Al Shabab la Somalia ambalo nalo pia hutekeleza mahsambualizi ya mara kwa mara katika nchi jirani. Makundi hayo ya kigaidi yanalenga kuchukua madaraka katika nchi za Afrika ili  kueneza idiolojia yao ya ukufurishaji katika nchi za bara hilo hasa Nigeria, Mali na Somalia.

Ingawa katika miaka ya hivi karibuni vita dhidi ya ugaidi ni nara ya viongozi wa  nchi mbali mbali za Afrika na pia madola ya Magharibi yanatumia kisingizio cha ugaidi kuingiza askari wao katika nchi mbali mbali za bara hilo lakini la kusikitisha ni kuwa ugaidi unazidi kuongezeka.

Baada ya kutimuliwa magaidi katika baadhi ya maeneo kadhaa ya eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, sasa magaidi hao wamelekeza jinai zao katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la sahara.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Nigeria imeshuhudia mashambulizi ya magenge yanayoshambulia shule na kuwateka nyara wanafunzi. Aidha katika maeneo mbali mbali ya Nigeria kumeshuhudiwa mashambulizi ya makundi ya kigaidi ambayo yamepelekea idadi kubwa ya watu wasio na hatia kuuawa.

Eneo la Borno, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria limetajwa kuwa ngome ya magaidi wa Boko Haram

Baada ya kushindwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika eneo la Asia Magharibi kuna ushahidi unaoonyesha kuwa magaidi hao sasa wanahamia katika nchi za Afrika. Tahadhari kadhaa zimetolewa kuhusu tukio hilo lakini hakuna hatua  imara zilizochukuliwa kuzuia magaidi hao wa ISIS kujipenyeza Afrika.

Jordan Coup mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema  makundi ya kigaidi barani Afrika yamevuruga sekta za uchumi, siasa na siasa.

Kati ya sababu ambazo zimepelekea kuongezeka ugaidi barani Afrika zimetajwa kuwa ni pamoja na kukosekana ushirikiano wa kutosha baina ya vikosi vya usalama vya nchi za bara hilo  na pia ukosefu wa bajeti ya kutosha ya vikosi hivyo.  Halikadhalika sababu nyingine ya ongezeko la ugaidi barani Afrika imetajwa kuwa ni uingiliaji wa madola ya Magharibi hasa Marekani, Ufaransa na Uingereza ambazo zimetuma askari katika nchi za Afrika kwa kisingizio cha  kukabiliana na ugaidi lakini  ni wazi kuwa zinafuatilia malengo ya kisiasa na kiuchumi.

Aidha ugaidi barani Afrika unatokana na ongezeko la umasikini na hali mbaya ya kiuchumi katika nchi nyingi za Afrika na hivyo makundi ya kigaidi yanatumia hali hiyo kujipenyeza kwa kuwalipa wapiganaji kiasi kikiuubwa cha fedha. Vile vile itikadi potovu ya ukufurishaji ya Uwahhabi imetajwa kuwa ni moja ya sababu ambazo zimeplekea kuongezeka ugaidi barani Afrika.

Magaidi wa Al Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya kuvizia mjini Mogadishu Somalia

Katika upande mwingine baadhi ya makundi ya kigaidi yanapata uungaji mkono wa siri wa nchi za kigeni na hivyo madola ya magharibi kwa kisingizo cha kukabiliana na ugaidi yanaeneza satwa yao katika nchi za Afrika. Ni kwa msingi huo ndio tunaona nchi kama Ufaransa imetuma askari wake katika eneo la Sahel la Magharibi mwa Afrika. Ni wazi kuwa lengo la askari hao wa Ufaransa ni kupora utajiri wa nchi za eneo hilo hasa madini ya urani, dhahabu na mafuta. Sera hiyo inafuatwa na madola mengine ya Magharibi yanayodai kukabiliana na ugaidi barani Afrika.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Maplecroft ya Uingereza ugaidi unazidi kushadidi barani Afrika na hata maeneo ambayo zamani hayakuwa na ugaidi sasa kunashuhudiwa ugaidi.

Kuongezeka makundi ya kigaidi Afrika kunapaswa kuwa kengele ya hatari si tu kwa nchi bara hilo bali kwa dunia nzima. Ongezeko la ugaidi ni tishio kubwa kwa usalama wa dunia na hivyo kuna haja ya kuwepo ushirikiano wa kimataifa na baina ya nchi zote za Afrika ili kuangamiza makundi hayo ya kigaidi.

Tags