Jun 10, 2021 12:28 UTC
  • Fatou Bensouda
    Fatou Bensouda

Kwa mara nyingine tena, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amewataka maafisa wa serikali ya Sudan kuwakabidhi watuhumiwa wa jinai za kivita katika eneo la Darfur kwa mahakama hiyo, akiwemo rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir.

Fatou Bensouda alitoa mwito huo jana Jumatano mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakati akiwasilisha taarifa yake ya mwisho kama Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC. Bensouda anamaliza muhula wake wa kuhudumu tarehe 15 mwezi huu wa Juni.

Katika hotoba hiyo, Bensouda amesema kufunguliwa ukurasa mpya wa uongozi nchini Sudan na kukabidhiwa mahakama hiyo ya mjini Hague nchini Uholanzi mtuhumiwa wa kwanza wa jinai za Darfur kunawapa matumaini makubwa.

Hali kadhalika Bensouda ametilia mkazo udharura wa kudhaminiwa usalama mashahidi katika faili la jinai za Darfur.

Bensouda ameliambia Baraza la Usalama la UN kwamba: "Waathiriwa na manusuru wa jinai za Darfur niolioongea nao wiki iliyopita wana ujumbe mmoja tu; kwamba Serikali ya Mpito ya Sudan iwakabidhi kwa ICC washukiwa watatu wa jinai za Darfur inaowazuiliwa, ambao ni rais wa zamani Omar al-Bashir, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Abdel Raheem Hussein, na aliyekwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Gavana, Ahmad Harun."

Picha inayoashiria ukubwa wa jinai za Darfur za mwaka 2003

ICC inamtuhumu Omar al Bashir kwamba alihusika na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo la Darfur huko Magharibi mwa Sudan na vilevile kutenda jinai dhidi ya binadamu na tayari imekwishatoa waranti wa kutiwa nguvuni mtuhumiwa huyo na wenzake. 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, watu zaidi ya laki tatu waliuawa katika machafuko ya Darfur yaliyoanza mwaka 2003 na wengine milioni mbili na nusu wamelazimika kuwa wakimbizi.

Tags