Jun 11, 2021 02:13 UTC
  • Ripoti: Watu 350,000 wamekumbwa na baa la njaa huko Tigray nchini Ethiopia

Kamati ya ngazi ya juu inayoongozwa na UN ambayo inajihusisha na kutafuta majibu ya haraka kwa mizozo ya kibinadamu inakadiria kwamba, karibu watu 350,000 katika mkoa wa Tigray uliokumbwa na vita huko Ethiopia wanasumbuliwa na baa la njaa.

Idadi hiyo iliwasilishwa katika mkutano Jumatatu wa Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Misaada ya Kibinadamu inayojumuisha mashirika 18 ya Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika yasiyo ya UN iliyoongozwa na mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock.

Uchambuzi huo uligundua kwamba, mamilioni ya watu wa Tigray wanahitaji "msaada wa haraka wa chakula na misaada ya sekta ya kilimo na maisha ili kuepusha uwezekano wa kutumbukia zaidi kwenye baa la njaa.

Hata hivyo mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia na Kukabiliana na Maafa nchini Ethiopia, Mituku Kassa, alisema jana Alhamisi kwamba kutangaza baa la njaa katika eneo la Tigray halitakuwa jambo sahihi. Kassa ameishutumu harakati ya Tigray People's Liberation Front (TPLF) kuwa inashambulia misafara ya misaada.

Tigray, Ethiopia

Amesema Ethiopia haina uhaba wowote wa chakula kuongeza kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya watu wa Tigray wamepewa msaada ya kutosha.

Jumatano iliyopita msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric alisema kwamba wafanyakazi wa UN wanaotoa huduma huko Tigray wameripoti matukio ya kuzuiliwa misaada, kuhojiwa, kushambuliwa, na kuwekwa kizuizini wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu katika vituo vya ukaguzi vya jeshi la Ethiopia. Amesema kuwa kumekuwapo pia na uporaji wa mali na misaada ya kibinadamu.

Ijumaa iliyopita, Mark Lowcock alionya kwamba, njaa inalinyemelea eneo la Tigray na Kaskazini mwa Ethiopia, akisema kuna hatari mamia ya maelfu ya watu au zaidi watafariki dunia kutokana na janga hilo.

Tags