Jun 12, 2021 07:51 UTC
  • Wakimbizi 9,000 kutoka Msumbuji wamerejeshwa kwa nguvu nyumbani kutoka Tanzania

Nchini Msumbiji katika mji wa pwani wa Palma jimboni Cabo Delgado bado wananchi wanaripoti kusikia milio ya risasi kila uchao, nyumba zao zikitiwa moto na hivyo kulazimika kukimbia maeneo mengine ndani ya nchi yao au hata kuvuka mpaka na kuingia Tanzania, hali inayoendelea kutia hofu kubwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kuhusu usalama wao.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi amewaambia waandishi wa habari Ijumaa kuwa mashambulizi yanafanywa na watu wenye silaha na kwamba  maelfu ya watu wanakimbia makazi yao, miezi miwili na nusu baada ya mashambulizi mengine ya kikatili kwenye eneo hilo kutoka makundi hayo.
Watu elfu 70 wamekimbia mji wa Palma tangu tarehe 24 mwezi Machi mwaka huu na kufanya idadi ya watu waliokimbia jimbo la Cabo Delgado kufikia 800,000.
Babar Baloch amesema UNHCR inaendelea kusisitiza wakimbizi wa ndani wapatiwe ulinzi na msaada nchini Msumbiji na wale walio hatarini zaidi na wanasaka usalama nchi jirani ya Tanzania wapatiwe hifadhi.

Hatahivyo, wakimbizi wengine wengi wameripotiwa kujaribu kuvuka mto Ruvuma ambao ndio mpaka na Tanzania kusaka hifadhi ya kimataifa, lakini kwa mujibu wa mamlaka za mpakani nchini Msumbiji zaidi ya wakimbizi 9,000 wamerejeshwa kinguvu nyumbani kutoka Tanzania kupitia kituo cha mpakani cha Negomano tangu mwezi Januari mwaka huu.
Wengine 900 wamerejeshwa Msumbiji kati ya tarehe 7 na 9 mwezi huu wa Juni wakiwa katika hali mbaya na wengine wametangana na familia zao.