Jun 12, 2021 12:43 UTC
  • Wanakijiji 90 wauawa katika shambulio la wabeba silaha Nigeria

Watu wasiopungua 90 wameuawa baada ya genge la watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia kijiji kimoja huko Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.

Msemaji wa Polisi katika eneo hilo ameliambia Shirika la Habari la Nigeria (NAN) kuwa, watenda jinai hao waliwashambulia wanakijiji nyakati za usiku katika kijiji cha Kadawa, mji wa Zurmi, jimboni Zamfara. Amesema ukatili huo ulifanyika usiku wa kuamkia jana Ijumaa.

Hapo jana, Gavana wa jimbo la Zamfara, Bello Matawalle aliwataka wananchi kujichukulia sheria mikononi na kukabiliana na magenge ya waasi wanaobeba silaha, wezi wa mifugo na makundi ya kigaidi yanayowahangaisha.

Wiki iliyopita, wezi wa mifugo waliua watu wasiopungua 88 katika vijiji saba katika jimbo la Kebbi lililoko katika eneo hilo hilo la Kaskazini Magharibi mwa Nigeria. 

Magenge ya wahalifu nchini Nigeria yameshadidisha hujuma katika pembe mbalimbali za nchi, ambapo mbali na wizi wa mifugo kumeshuhudiwa pia ongezeko kubwa la utekaji nyara wanafunzi wa shule.

Ghasia za umwagaji damu jimboni Zamfara

Kwa upande mwingine pia, kundi la kigaidi la Boko Haram linaendelea kufanya hujuma za hapa na pale hususan katika jimbo la Borno, la kaskazini mashariki mwa nchi.

Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS). 

Tags