Jun 13, 2021 02:50 UTC
  • Polisi ya Nigeria yafyatua gesi ya kutoa machozi katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia

Polisi wa Nigeria wamefyatua gesi ya kutoa machozi kutawanya waandamanaji wanaopinga serikali huko Lagos na katika mji mkuu, Abuja, na ripoti zinasema kuwa baadhi ya wanaadamanaji hao wakamatwa na wengine kujeruhiwa.

Maandamano hayo ya kitaifa yaliitishwa jana Jumamosi na wanaharakati katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia, ambayo inakumbusha tukio la Nigeria kuelekea kwenye utawala kiraia zaidi ya miaka 20 iliyopita. Waandamanaji hao wamekosoa kile wanachosema ni utawala mbaya, ukosefu wa usalama, na pia marufuku ya hivi karibuni ya utumiaji wa mtandao wa Twitter iliyotangazwa na serikali ya Rais Muhammadu Buhari.

Maandamano kama hayo pia yameshuhudiwa katika miji mingine kadhaa ya Nigeria kama Ibadan, Osogbo, Abeokuta na Akure, huko Kusini Magharibi mwa Nigeria.

Maandamano hayo yalikuwa ya kwanza kufanyika katika miji kadhaa ya Nigeria tangu harakati ya "#EndSARS" dhidi ya ukatili wa polisi mnamo Oktoba mwaka jana ilipobadilika na kuwa harakati kubwa zaidi ya kupinga serikali katika historia ya sasa ya Nigeria.

Mamia ya waandamanaji waliokusanyika katika jiji lenye wakazi zaidi ya milioni 20 la Lagos, walifyatuliwa gesi ya kutoa machozi na kutawanyika huku na kule. Waandamanaji hao walibeba mabango yaliyosema "Buhari Lazima Aondoke" na kutaka mageuzi nchini Nigeria.

Waandamanaji wengine pia walibeba mabango yanayotaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi nayeshikiliwa mahabusu kwa miaka mingi sasa wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeia (IMN).

Buhari, jenerali wa zamani aliyechaguliwa mara ya kwanza kuwa rais wa Nigeria mwaka 2015, amekuwa chini ya mashinikizo makubwa kutokana na kuongezeka hali ya ukosefu wa usalama katika taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, ambalo lina watu zaidi ya milioni 200.

Maandamano ya Jumamosi ya jana yaliitishwa sambamba na maadhimisho ya "Siku ya Demokrasia", ya kumbukumbu ya kuchaguliwa Moshood Kashimawo Abiola kuwa rais wa Nigeria mnamo 1993.

Ushindi wa Abiola ulifutwa na serikali ya kijeshi ya wakati huo, suala ambalo liliitumbukiza Nigeria katika machafuko ya kijamii ya miezi kadhaa.

Nigeria ilirudi kwenye utawala wa kiraia mwezi Mei 1999, lakini Buhari alichagua Juni 12 kama Siku ya Demokrasia baada ya kuwa rais, ili kumuenzi Abiola na mashujaa wengine wa mapambano ya demokrasia.

Tags