Jun 13, 2021 11:23 UTC
  • Watunisia waandamana kupinga ukandamizaji wa polisi; ghasia zaibuka

Duru za kuaminika zimetangaza kuwa, wananchi wa Tunisia wamekabiliana na polisi na kuibua ghasia baada ya maandamano yaliyofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis kupinga serikali, ukandamizaji na vitendo vya ukatili vya polisi ya nchi hiyo.

Makumi ya wanaharakati wa mrengo wa kushoto na wakazi wa maeneo yenye msongamano wa watu katika mji mkuu Tunis jana jioni waliandamana hadi mbele ya jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo huku wakiwa wamebeba mabango na vitambaa vyenye maandishi yanayoilaani polisi ya nchi hiyo. Baadhi ya mabango hayo yalikuwa na maandishi yanayosema: "Nani atatulinda mkabala wa polisi?" na "okoa maisha, mhukumu polisi."  

Aidha jana usiku mamia ya vijana wa Kitunisia walikabiliana na polisi karibu na kituo cha upekuzi cha cha eneo la Sidi Hassine nje kidogo ya mji wa Tunis wakilalamikia ukandamizaji unaofanywa na jeshi la polisi dhidi ya raia. Hayo ni kufuatia ukandamizaji unaofanywa na polisi dhidi ya raia wa maeneo hayo baada ya mwanaume mmoja kufariki dunia akiwa katika seli ya polisi. 

Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu ya Tunisia (LTDH) imeeleza kuwa, ghasia na machafuko ya jana ni mwendelezo wa maandamano yaliyofanywa kwa siku tatu mtawalia  baada ya kuaga dunia raia huyo katika mazingira ya kutatanisha. Mtu huyo aliaga dunia Jumanne iliyopita baada ya kutiwa nguvuni na polisi akishukiwa kujishughulisha na biashara ya mihadarati. 

Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Tunisia imetoa taarifa ikilamu ghasia na ukandamizaji unaofanywa na polisi dhidi ya wananchi kwa lengo la kunyamazisha sauti za waandamanaji. Vilevile imemlaumu Waziri Mkuu wa Tunisia, Hichem Mechichi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia kwa utendaji wake mbaya. Mechichi amekanusha tuhuma hizo.

Hichem Mechichi, Waziri Mkuu wa Tunisia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani