Jun 13, 2021 11:45 UTC
  • Sameh Shoukry
    Sameh Shoukry

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeishitaki Ethiopia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mzozo wa pande tatu juu ya ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry ameliandikia barua baraza hilo akilalamikia uamuzi wa Ethiopia wa kuendelea kujaza maji katika Bwawa la Reinassance na namna Cairo inavyopinga hatua ya Addis Abab ya kuzitishwa sera zake nchi za Misri na Sudan kupitia hatua za upande mmoja na kukiuka sheria za kimataifa. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Ahmad Hafidh amesema kuwa, barua ya Shoukry ni uthibitisho rasmi mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Mawaziri wa Wizara za Mambo ya Nje na Maji za Misri hivi karibuni walifanya ziara huko Sudan na kuzungumza na wenzao wa nchi hiyo kuhusu taathira ya hatua hasi za Ethiopia za kuendelea kujaza maji katika Bwawa la Reinassance. 

Bwawa la Reinassance lililojengwa na Ethiopia juu ya Mto Nile katika ardhi ya nchi hiyo 

Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambao umegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji ya nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje. Mzozo huo umezusha wasiwasi wa kutokea vita na mapigano baina ya nchi hizo tatu.

Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri ametishia kwamba "Cairo itatoa jibu lisilotasawarika iwapo nchi yake itapata madhara kutokana na Bwana la Renaissance linalojengwa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile."

Rais wa Misri alisisitiza kuwa maji ya Misri ni mstari mwekundu na anayetaka kujaribu atakiona cha mtemakuni. 

Ethiopia kwa upande wake imejibu vitisho hivyo ikisema iko tayari kukabiliana na hujuma ya aina yoyote ya adui.